Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ni mojawapo kati ya miji mikongwe Tanzania. Ilianzishwa mnamo karne ya 11 na wafanyabiashara wa kiarabu. Kipindi cha ukoloni wa mwingereza, wafanyabiashara wa kihindi waliishi sehemu nyingi za mijini katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwa mojawapo ni Lindi. Jina hili la Lindi maana yake ni SHIMO REFU, ilianzishwa miaka ya 1700 kama bandari ya kusafirisha watumwa na pembe za ndovu. Misafara ya watumwa kutoka Ziwa Nyasa iliishia katika bandari hii, Hadi miaka ya 1950 Lindi ilikuwa mahali pazuri kwa maisha ukianza na waarabu walioishi karne ya 18 wakifuatiwa na watu wa bara dogo la India, baadaye wakaja wajerumani hatimaye wakamalizia waingereza. Wakati wa nusu ya kwanza ya karne ya 20 nyumba nyingi za kuvutia zilijengwa katika mwambao wa Lindi.
Mji wa Lindi upo katika mdomo wa mto Lukuledi ukizungukwa na milima inayotazama bahari ya Hindi. Mtwara ikawa mji uliopoteza sifa ya Lindi kwa sababu ya kuwa na bandari muhimu na soko zuri katika mwambao wa Kusini, lakini bado sifa nzuri ya Lindi kuwa sehemu bora ya utalii inaendelea. Pamoja na kuwa na watu wachache wanaoweza kuzungumza lugha ya kiingereza, watu wengi ni wakarimu na wako tayari kusaidia kwa namna inavyohitajika na wageni.
Lindi Mjini ilikuwa kama kituo cha utawala kwa upande wa jimbo la Kusini hadi mwaka 1952 ambapo shughuli nyingi za utawala zilihamishiwa Mtwara. Kuhama kulitokana na hali nzuri ya bandari ya Mtwara na mazingira yenye ardhi nzuri ya Mtwara. Matokeo yake ikawa ni maendeleo duni ya kiuchumi na ukuaji mdogo wa idadi ya watu katika mji wa Lindi. Mwaka 1971 Lindi mjini ikawa makao makuu ya huduma za utawala na biashara hatimaye mji ukaanza kubadilika taratibu sana ambapo kiuhalisia mabadiliko hayo hayakuweza kuonyesha tofauti ya kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Mwaka 1972, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianzisha sera ya kupeleka madaraka mikoani. Hii ikapelekea kufifisha ukuaji wa Halmashauri za mijini bali ilikazia maendeleo vijijini, hatimaye miundombinu na maendeleo ya mijini vikafifia. Hivyo Serikali ikarudisha tena Halmashauri za mijini. Kiujumla wakati wa utawala wa wakoloni mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma ilikuwa ni jimbo moja la Kusini. Baada ya uhuru utwala wa majimbo ukafa na kuundwa utawala wa mikoa. Lindi na Mtwara ikawa mkoa mmoja hadi mwaka 1971 ambapo Lindi na Mtwara ikawa mikoa ya kujitegemea kila mmoja na utawala wake.
Municipal Director
Anuani ya Posta: 1070 Lindi
Simu: +255232202164
Simu ya mkononi: +255767042958
Barua Pepe: info@lindimc.go.tz
Hakimiliki @2020 Manispaa ya Lindi. Haki zote zimehifadhiwa