Mkuu wa Wilaya ya Lindi Ndugu Shaibu Ndemanga ametoa siku saba kwa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kuhakikisha miradi yote inaendelea kwa kasi,kwani imeonekana kusuasua.Ameyasema hayo leo kwenye kikao kazi kilichojumuisha Manispaa ya Lindi na Halmashauri ya Mtama kilichofanyika ukumbi wa Mikutano wa Mkurugenzi wa Manispaa.
Aidha,amewataka wataalamu wanaohusika na miradi hiyo kuhakikisha wanasimamia vyema miradi hiyo huku ikikidhi ubora na viwango vinavyotakiwa kwa majengo ya serikali huku ikiendana na thamani ya fedha inayotolewa kutekeleza miradi hiyo.
Vilevile,Ndemanga amemuagiza Mkurugenzi kuteua wahandisi watakaokuwa wanakaa kwenye miradi muda wote wa utekelezaji wa miradi hiyo mpaka itakapokamilika lakini pia kupatiwa taarifa za miradi hiyo kila siku jioni ili aweze kujua maendeleo na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Mkuu wa Wilaya amewataka watumishi kutokufanya biashara kama wazabuni na Manispaa kwani inawafanya kuwa bize na biashara zao binafsi na kuacha kufanya kazi za serikali walizopangiwa.
Mkurugenzi wa Manispaa Ndugu Juma Mnwele ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya na kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wote.Pia amesisitiza watumishi kuacha kufanya biashara na Manispaa kitu ambacho kinapelekea wafanyabiashara wenye kampuni kutokufanya biashara.
Mnwele amewataka watumishi wa idara na vitengo vinavyohusika na utekelezaji wa miradi hiyo kubadilika lakini pia kufanya kazi kwa bidii na nidhamu ili kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa vyema lakini pia kujengwa kwenye ubora unaotakiwa.
Municipal Director
Anuani ya Posta: 1070 Lindi
Simu: +255232202164
Simu ya mkononi: +255717469888
Barua Pepe: info@lindimc.go.tz
Hakimiliki @2020 Manispaa ya Lindi. Haki zote zimehifadhiwa